Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), inatarajia kuvifuta vituo 155 vinavyotoa mafunzo ya elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi maarufu kama QT kutokana na kukiuka taratibu zilizowekwa na kushindwa kufuata masharti ya usajili.
Naibu Mkurugenzi Taaluma wa taasisi
hiyo, Dk Kassim Nihuka aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mpango wa utoaji elimu ya
sekondari nje ya mfumo rasmi kwa njia ya mafunzo ya jioni.
Dk Nihuka alisema miongoni mwa masharti
yaliyokiukwa na vituo hivyo ni kutokulipa ada ya uratibu ambayo ni Sh
20,000 kwa kila mwanafunzi aliyesajiliwa na vingine mazingira yake ya
kufundishia hayaridhishi.
Alisema kutokana na hali hiyo, taasisi
hiyo imetoa muda kwa waendeshaji wa vituo hivyo ili warekebishe kasoro
hizo na ifikapo Machi mosi mwaka huu kama hawajazishughulikia changamoto
zao, vituo hivyo vitafungiwa.
Dk Nihuka alisema mpaka sasa kuna vituo
420 nchi nzima vinavyotoa mafunzo ya elimu ya sekondari nje ya mfumo
rasmi, na kati ya hivyo, vituo 337 ni vya wadau na 83 vinasimamiwa na
TEWW.
Alisema kati ya hivyo, vituo 182
vimesajiliwa na vimefuata taratibu zinazotakiwa, lakini vituo 155
vimekiuka taratibu hivyo viko hatarini kufutwa kutokana na kukiuka
taratibu zinazotakiwa.
“Programu hii ambayo inaendeshwa katika
majengo ya shule za msingi na sekondari za serikali ni vituo 83 na shule
za wadau mbalimbali 337 nchini zimewanufaisha vijana na watu wazima
95,140 tangu mwaka 2010 hadi 2016,” alieleza Naibu Mkurugenzi huyo.
Pia alisema kwa wanafunzi wanaosoma
katika mfumo huo wenye miaka chini ya 23 wakimaliza elimu ya kidato cha
nne na kufaulu vizuri ana fursa ya kuendelea na masomo kama wanafunzi
wengine ya kidato cha tano na sita, lakini mwenye miaka zaidi ya 25
atasoma kwa mwaka mmoja kidato cha tano na sita.
0 comments:
POST A COMMENT